Watu 26 washambuliwa na mbwa Mwananyamala


Wakazi 26 wa Wilaya ya Kinondoni wakiwemo watoto wameshambuliwa na kujeruhiwa na mbwa anayedaiwa ana kichaa alipokuwa akizurura maeneo ya Mwananyamala.

Kati ya waliong'atwa wapo watoto 20 wa kuanzia miaka minne hadi 12 na watu wazima sita, ambao ni wakazi wa mitaa ya Kambangwa, Kinondoni na Mwananyamala kwa Kopa.

Akizungumza leo Jumamosi Machi 9,2024 na Mwananchi Digital, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Manispaa ya Kinondoni, Aquilinus Shiduki amesema mbwa huyo na wengine wawili tayari wameshauliwa katika msako wa kumtafuta baada ya kufanya tukio hilo.

“Ni kweli tukio hilo lilitokea jana kwa watu kushambuliwa na mbwa huyo, lakini baada ya kuripotiwa, msako mkali ulifanyika jana na kufanikiwa kumkamata na kumuua.
“Katika msako huo ambao ni endelevu, leo tena tuliwakamata mbwa wengine wawili waliokutwa wakizurura, maofisa wetu wa wanyama wakawaua na kufanya mbwa waliouawa hadi sasa kufika watatu,”amesema Shiduki.
Kutokana na tukio hilo, amewatahadharisha watu wenye kufuga mbwa kuzingatia sheria ya wanyama ya mwaka 2008 kuhakikisha kama wana mifugo yao wahakikishe wanawafungia ndani kwa kuwa wanapotoka ndipo wanasababisha madhara kama hayo.

“Kwa hali iliyopo ina maana mbwa akionekana anazurura tutamshughulikia kwa namna yake ili kuepusha yasije kutokea tena yaliyotokea,”amesema mkuu huyo wa kitengo cha mawasiliano.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Zavery Benela amesema walianza kupokea majeruhi wa tukio hilo kuanzia jana (Ijumaa) saa 10:30 jioni hadi saa 4:30 usiku.
Amesema jumla ya watu waliofika walikuwa 22 na wengine wanne wamefika hospitalini hapo leo (Jumamosi).

Akielezea hali zao, amesema wote wanaendelea vizuri kwa kuwa walipofika walitibiwa kwa kupatiwa chanjo tiba na chanjo kinga.

Pia, amesema chanjo tiba wataendelea kuwapa kwa siku tatu tangu walipojeruhiwa, siku ya saba, ya 14 na ya 28.

Amesema kati ya majeruhi hao 26, waliojeruhiwa vibaya walikuwa watatu huku mama mmoja alijeruhiwa sana kwa kuwa alikuwa kipambana na mbwa huyo ili asimng’ate.

Pia, amesema alikuwepo mtoto aliyeng’atwa karibu na jicho na mtoto mwingine aling’atwa kwenye paja na kutoa damu nyingi, lakini wote walihudumiwa na kuruhusiwa.

“Majeruhi wote waliofika hapa tuliowahudumia na hata watakaofika tutatafanya hivyo, nawasihi waliokumbwa na kadhia hiyo wasisite kuja kupata matibabu na yatakuwa bure,” amesema Dk Benela.

Baadhi ya wazazi wa watoto ambao wamejeruhiwa na mbwa huyo akiwamo wa Rehema Said, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Msisiri, amesema ilikuwa saa tisa wakati mtoto wake na wenzake wanne wakiwa wanatoka shule, mbele yao wakamuona mbwa na kuanza kumkimba.

Amesema lakini kwa bahati mbaya mbwa alimshika sketi yake na kuanza kumng’ata mkononi na kwenye makalio huku wenzake wakifanikiwa kumkimbia.

Fatma Hamis, ambaye ni mzazi wa Rehema na mkazi wa Mwananyama kwa Makoma, amesema binti yake huyo alirudi nyumbani majira ya mchana akiwa analia.

Amesema marafiki zake waliokuwa wamemsindikiza walimwambia kuwa ameng’atwa na mbwa na hapo ndipo wakamkimbiza hospitali.

Katika ushauri wake, Fatma ameomba mmiliki wa mbwa atafutwe ili aweze kuwalipa fidia kwa madhara ambayo wameyapata watoto wao na kuchukuliwa zaidi hatua za kisheria kutokana na kutofungia mnyama wake huyo.

Joseph Mapunda, mwenye mtoto wa miaka minne amesema jana wakati tukio linatokea ilikuwa saa kumi jioni akiwa anangalia mpira sebuleni kwake ndipo alisikia mtoto wake nje akiwa analia.
Mapunda amesema alipotoka alimkuta mkono mtoto wake ukiwa umeshikiliwa na mbwa na hapo ndipo wakaanza kumuokoa kisha kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala kupata matibabu.

"Nilikuwa nimekaa sebuleni, nafuatilia mpira, mara nje nikasikia mtoto analia sana na nilipotoka kujua kafanya nini namkuta mbwa kaung'ang’ania mkono wake kwa kweli ilinishtua sana na kuona huyo hawezi kuwa mbwa wa kawaida,"amesema Mapunda.

Mapunda ameomba hatua kali zichukuliwe dhidi ya wanaoachia wanyama hao kuzurura ovyo kwa kuwa mpaka sasa inawaumiza kichwa hawajui kama huyo mbwa alikuwa na kichaa au la.

Jamila Maliki, amesema katika tukio hilo, mjukuu wake mwenye miaka minane aling’atwa mgongoni alipotoka nje barazani kumuokoa mdogo wake wa miaka mitatu wakati mbwa huyo alipokuwa akimshambulia.

“Wakati mjukuu wangu huyo alipotoka kumuokoa mdogo wake alimrukia mwenzake na hapo mbwa ndipo alipomng’ata mgongoni,”ameelezea Jamila.

Hata hivyo, ameshukuru wote waliofika hospitalini waliweza kupata huduma nzuri na kueleza kuwa wameandikiwa tarehe za kurudi.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post